Zijue kanuni muhimu za ufugaji wa kuku
Zijue kanuni muhimu za ufugaji wa kuku
Wafugaji wengi nchini hujihusisha na ufugaji wa kuku kwa lengo la kujipatia chakula na kipato.
Kipato hicho hutokana na mauzo ya mazao yatokanayo na ufugaji wa kuku kama vile mayai, nyama na mbolea
Pamoja na faida hizo, lakini wafugaji wengi wamekuwa hawafuati kanuni na mifumo sahihi kwa ajili ya ufugaji wa kuku.
Mifumo ya ufugaji wa kuku?
Kuna aina tofauiti za mifumo ya ufugaji wa kuku. Kwa Tanzania, inayotumika ni mfumo huria, nusu huria na shadidi. Huria ni kuwaacha kuku nje wakijitafutia chakula na kurudi bandani jioni. Nusu huria ni kuwafuga bandani na kisha kuwatoa nje baadhi ya nyakati, wakati shadidi ni kumfuga kuku ndani ya banda.
Kanuni zinazoongoza ufugaji wa kuku
Ufugaji wa kuku utakuwa endelevu na wenye tija kwa mfugaji endapo
atafuata kanuni maalumu kama kuwa na banda bora kwa ajili ya
ufugaji wa kuku, uchaguzi wa mbegu bora ya kuku, matunzo ikiwa ni pamoja na kulisha kuku kulingana na hatua mbalimbali za ukuaji.
Kanuni nyingine ni udhibiti wa magonjwa ya kuku kwa wakati na kutunza kumbukumbu kwa kila hatua.
Banda la kuku na sifa zake
Kuku wanahitaji kuwa na banda bora. Hii itasaidia wasipate madhara ya
aina yoyote kama vile kushambuliwa na wanyama au magonjwa ya kuambukiza.
Sifa za banda la kuku ni pamoja na kuwa imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kuku dhidi ya hali ya hewa hatarishi. Banda liwe na mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi. Jenga banda sehemu yenye mwinuko isiyotuamisha maji. Banda liwe sehemu isiyo na upepo mkali na iwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi. Hakikisha banda lina vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala. Banda liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea vifaranga. Hakikisha banda lina nafasi ya kutosha kulingana na idadi ya kuku. Weka vyombo vya chakula na maji kwenye banda kwa mpangilio. Ni muhimu kuhakikisha kuwa kwenye mazingira ya joto, banda lina ukuta mfupi na sehemu kubwa iwe wazi yenye wavu. Kwenye mazingira ya baridi, banda liwe na ukuta mrefu unaokaribia paa.
Vifaa kwa ujenzi wa banda bora
Vifaa vya ujenzi wa banda la kuku vinatofautiana kulingana na maeneo
na uwezo wa mfugaji. Ni muhimu kujenga banda kwa kuzingatia gharama na upatikanaji wa vifaa katika eneo husika. Vifaa vinavyohitajika kwa kila banda ni sakafu, kuta, paa na uzio
Ukubwa wa banda
Ukubwa wa banda utategemea idadi ya kuku na aina ya kundi la kuku.
Kuku wanahitaji nafasi tofauti kutegemeana na umri, aina na njia ya ufugaji. Eneo la mita moja ya mraba linatosha kwa vifaranga 16 wa umri wa wiki moja hadi nne, hivyo banda lenye mita za mraba 16 linaweza kulea vifaranga 320 hadi wiki ya nne. Baada ya wiki ya nne eneo hili liongezwe kutegemea aina ya kuku na
njia inayotumika katika ufugaji
Idadi ya kuku kwa mita moja ya mraba
Kuku wa umri wa siku moja hadi wiki nne wakiwa wa mayai au wanyama wanapaswa kuwa 18. Kuanzia wiki ya tano hadi ya nane punguza wabaki kuku tisa.
Hakuna maoni: